Habari Za Kimataifa

Kusini Riek Machar na mke wake Wakutwa na Maambukizi ya Corona
Kusini Riek Machar na mke wake Wakutwa na Maambukizi ya Corona

Makamu Rais wa kwanza wa Sudani Kusini Riek Machar na mke wake Angelina Teny wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Dkt. Machar alisema kwamba yeye na mke wake ambaye pia ni waziri wa ulinzi, wamepata maambukizi baada ya kutangamana na jopo la ngazi ya juu la kukabiliana na virusi hivyo nchini humo.

Machar amesema kwamba hana dalili zozote na hali yake ya afya iko sawa lakini atajiweka karantini kwa siku 14.

Wengine waliothibitishwa kuambukizwa ni walinzi kadhaa na wafanyakazi.

Mpaka sasa Sudan Kusini imerekodi waathirika 236 na vifo vinne.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake: "Bado tunasubiri matokeo mengi na ni matumaini yetu kwamba kesho, tutakuwa na orodha kamili ya walioambukizwa katika jopo hili," Machar amezungumza hayo katika mkutano na wanahabari uliofanyika Jumatatu mjini Juba...Huenda daktari akatutembelea hadi atakapotuarifu kwamba wakati umewadia wa kumaliza karantini''.

May 19, 2020

Trump Anatumia chloroquine Kutibu magonjwa na kujikinga na Corona
Trump Anatumia chloroquine Kutibu magonjwa na kujikinga na Corona

Rais wa Marekani amesema anatumia dawa ya hydroxychloroquine ya kutibu Malaria, kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona.

Trump anatumia dawa hiyo licha ya onyo kutoka kwa serikali yake kwamba inatakiwa kutolewa tu kwa wagonjwa wa COVID-19 waliolazwa hospitalini ama kufanyiwa uchunguzi kutokana na uwezekano wa athari mbaya za dawa hiyo.

Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba amekuwa akitumia dawa hiyo pamoja na vidonge vya madini ya zinki kila siku, kwa muda wa wiki moja na nusu sasa.

Dawa hiyo hata hivyo inasemekana kuwa na athari kwa baadhi ya wagonjwa na haijaonyesha kuwa na uwezo wa kukabiliana na virusi vya corona.

Trump amesema daktari wake hakumuandikia dawa hiyo, lakini alimuomba daktari wa ikulu ya White House kumuandikia na kusema anaitumia kwa sababu anaamini ni dawa nzuri.

Rais huyo amekuwa akishinikiza matumizi ya dawa hiyo, ingawa bado hakuna utafiti mpana uliofanyika kuhusiana na uwezo wake katika kutibu COVID-19.

May 19, 2020

Kituo cha kudhibiti magonjwa cha AU chaitaka Tanzania kutoa takwimu Za Corona
Kituo cha kudhibiti magonjwa cha AU chaitaka Tanzania kutoa takwimu Za Corona

Kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kilichopo chini ya Umoja wa Afrika (AU) kimeitaka Tanzania kutoa takwimu mpya za mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini humo.

Mkurugenzi wa Africa CDC, Dkt John Nkengasong leo Alhamisi Aprili 14 amesema kuwa kituo chake kwa kutumia takwimu hizo kipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuipatia msaada wa kitaalamu na kiufundi unaohitajika.

"Hili ni janga kubwa kwa bara (Afrika) lote na dunia kwa ujumla… hivyo ni kwa faida ya Tanzania kutoa takwimu kwa wakati ili tufahamu mapungufu yapo wapi na tuwasiadie kadri itakavyohitajika," amesema Dkt Nkengasong katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao.

''Dawa ya Madagascar sio ya kugawanywa kwa Watanzania'', asema Kabudi

Kwa ujumla wake, Africa CDC imesema inazitaka nchi zote kutoa takwimu kwa haraka kwa kuwa hiko ndicho kiungo muhimu katika kuendesha vita dhidi ya mlipuko wa corona.

May 14, 2020

WHO imeonya kwamba virusi huenda vikabakia nasi.
WHO imeonya kwamba virusi huenda vikabakia nasi.

Janga la virusi vya corona huenda lisiondoke na watu duniani watalazimika kuishi nalo kama ilivyo kwa virusi vya HIV, shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya, wakati idadi ya watu waliofariki kutokana na janga hilo duniani ikikaribia kufikia 300,000.

Zaidi ya watu milioni 4.37 wameripotiwa kuambukizwa virusi vya corona duniani na watu 295,923 wamefariki kwa mujibu wa idadi iliyowekwa pamoja na shirika la habari la Reuters.

Maambukizi yameripotiwa katika zaidi ya nchi na maeneo 210 tangu kesi ya kwanza kugundulika nchini China Desemba mwaka 2019.

Marekani imeorodhesha zaidi ya vifo 1,800 jana, na kufikisha idadi ya watu waliofariki nchini humo kuwa 84,059. Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa tu akitupia lawama China , ambako ugonjwa huo umetokea mwishoni mwa mwaka jana.

May 14, 2020

Shirika la UNICEF latoa wito wa msaada wa dola bilioni 1.6 kwa ajili ya watoto
Shirika la UNICEF latoa wito wa msaada wa dola bilioni 1.6 kwa ajili ya watoto

Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limetoa wito wa mchango wa dola bilioni 1.6 hiyo ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya kiasi cha pesa ilichoitisha miezi miwili iliyopita ili kuwasaidia watoto wanaokumbwa na mizozo ya kibinadamu na ambao kwa sasa wanapambana na virusi vya corona.

UNICEF imesema kuanzia mwezi Machi, imepokea dola milioni 215. Watu milioni nne kote duniani wameathirika na virusi vya corona huku zaidi ya watu 282,000 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo wa mapafau.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linafanya kazi katika nchi ambazo zinakabiliwa na mizozo ya kibinadamu kwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona na kupunguza athari ya virusi hivyo kwa uwezo wa raia kupata matibabu, chakula, maji, elimu na ulinzi.

Utafiti wa UNICEF umeonyesha kwamba watoto bilioni 1.8 wanaishi katika mojawapo ya nchi 132 ambazo zina baadhi ya vikwazo vilivyowekwa na serikali kwa ajili ya kupambana na virusi vya corona.

May 12, 2020

Wagonjwa wa Corona Kenya Waongezeka,Madereva wa Malori mipakani wachangia asilimia kubwa
Wagonjwa wa Corona Kenya Waongezeka,Madereva wa Malori mipakani wachangia asilimia kubwa

Takwimu nchini Kenya zinasema kuna ongezeko la wagonjwa wapya 28 wenye Virusi vya Corona na kufanya idadi ya wagonjwa kufikia 700.

Kati ya wagonjwa hao 28 wapya 10 kati yao wanatoka Mombasa, 9 kutoka Kajiado na 7 kutoka Nairobi huku 2 wakitoka Wajir.

Wagonjwa wote 9 kutoka Kajiado ni madereva wa malori ya masafa marefu ambao walikuwa wanarudi kutoka Tanzania katika mpaka wa Namanga.

''Madereva wa Tanzania waliokuwa wakiingia Kenya kupitia mpaka huo wanapimwa upande wao wa eneo lao la mpakani. Madereva wa tano wa Tanzania pia walikutwa na virusi vya ugonjwa huo na tayari tumewasiliana na mamlaka ya taifa hilo kulishughulikia suala hilo'' Rashid Aman, Katibu Mtendaji Wizara ya Afya nchini Kenya.

May 12, 2020

Umoja wa Mataifa waomba dola bilioni 4.7 kupambana na janga la COVID-19
Umoja wa Mataifa waomba dola bilioni 4.7 kupambana na janga la COVID-19

Umoja wa Mataifa umetoa ombi jipya la dola bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwalinda mamilioni ya watu na kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya korona katika mataifa yaliyo na hali mbaya zaidi duniani.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinaadamu, Mark Lowcock, amesema kwamba machungu makubwa zaidi ya janga la COVID-19 yatakuwa mataifa yaliyo masikini zaidi duniani, na kwamba bila ya kuchukuwa hatua madhubuti hivi sasa, dunia inapaswa kujitayarisha kwa ongezeko la migogoro, njaa na umasikini.

Fedha hizo ni kando ya zile dola bilioni 2 ambazo tayari Umoja wa Mataifa ulikuwa umeziomba wakati ulipozinduwa mpango wake wa huduma za kibinaadamu tarehe 25 Machi.

Hadi sasa, umeweza tu kukusanya nusu ya kiwango hicho.

Idadi kamili ya dola hizo bilioni 6.7 kinatazamiwa kugharamia mpango wa huduma za kibinaadamu kutoka sasa hadi mwezi Disemba.

May 7, 2020

Poland yatangaza kusogeza mbele uchaguzi wa Rais
Poland yatangaza kusogeza mbele uchaguzi wa Rais

Chama tawala nchini Poland na mshirika wake katika serikali ya mseto wametangaza kufikia makubaliano ya kuahirisha uchaguzi wa rais uliopangwa Jumapili ijayo na kusema tarehe mpya itatanganzwa hivi karibuni.

Mkuu wa chama tawala cha PIS Jaroslaw Kaczynski na kiongozi wa chama kidogo cha kihafidhina kilicho sehemu ya serikali ya Poland , wameutaja uamuzi huo kuwa njia itakayotoa nafasi kwa kila raia kushiriki uchaguzi wa kidemokrasia.

Mei 10 ilikuwa tarehe ya uchaguzi iliyopangwa zamani lakini janga la virusi vya corona na vizuizi vilivyowekwa kukabilaina na kadhia hiyo, imefanya kuwa vigumu kwa Poland kuendelea na maandalizi ya uchaguzi.

Hapo kabla chama tawala kilinuwia kuendelea na uchaguzi Jumapili inayokuja kwa upigaji kura kufanyika kwa njia ya posta, lakini raia wengi nchini Poland walionya uchaguzi huo usingefanyika vizuri au kwa njia ya haki

May 7, 2020

Rais Trump Atoa Tumaini Upatikanaji Dawa ya Corona
Rais Trump Atoa Tumaini Upatikanaji Dawa ya Corona

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba ana matumaini kuwa Marekani itapata chanjo ya vurusi vya corona kabla ya 2021.

"Tuna uhakika kwamba tutapata chanjo kufikia mwisho wa mwaka huu," amesema wakati wa mazungumzo na kituo cha habari cha Fox News.

Hata hivyo alisema kwamba atakuwa ni mwenye furaha iwapo nchi nyengine itaipiku Marekani katika utafiti, na kuongeza: ''Sijali. Ninachotaka nikupata chanjo tu inayofanya kazi"

Wataalamu wengi wanasema huenda chanjo hiyo ikachukua miezi 12 hadi 18 kuwa tayari.

Wanasayansi kote duniani kwasasa wanajitahiji kutengeneza chanjo lakini wataalamu wengi wanatarajia kwamba itakuwa tayari sokoni kwa halaiki ya watu ifikapo 2021.

Trump alionekana kuwa na matumaini zaidi kuliko washauri kwa makadario ya ni lini dawa hiyo inaweza kupatikana kwa mara ya kwanza.

May 4, 2020

Wagonjwa Wa Corona Nchini Kenya Wafika 465Wapona 167
Wagonjwa Wa Corona Nchini Kenya Wafika 465Wapona 167

Wizara ya Afya Kenya imesema licha ya maambukizi ya jumla ya corona kuongezeka na kufikia 465 lakini wagonjwa wengine 15 wamepona na kufanya idadi ya waliopona corona kufikia 167 kutoka 152, ila kuna ongezeko la vifo viwili na sasa vifo vya corona Kenya ni 24.

Wizara ya Afya Kenya imesema wagonjwa wengine wa corona 30 wameongezeka na kufanya idadi ya jumla ya maambukizi kufikia 465 kutoka 43

“Tumewapima Watu 883 ndani ya saa 24 na kati yao 30 wamekutwa na corona, hii ni idadi kubwa kuwahi kutokea kwa siku tangu corona iingie Kenya”

May 4, 2020

Rais Trump azuia kwa muda uhamiaji Marekani
Rais Trump azuia kwa muda uhamiaji Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amezuia kwa muda uhamiaji nchini Marekani kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wa kimarekani kutokana na msukosuko wa kiuchumi uliosababishwa na janga la virusi vya Corona.

Hatua ya Trump imekuja wakati Umoja wa Mataifa umeonya kwamba ulimwengu unakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu.

Onyo la Umoja wa Mataifa limetolewa katika kipindi ambacho mataifa ya dunia yanapambana kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimewauwa watu 177,000 na wengine zaidi ya milioni 2.5 wameambukizwa.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP David Beasley ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana kwamba sio tu ulimwengu unakabiliwa na janga la kiafya bali pia janga kubwa la kibinadamu.

April 22, 2020

Papa Francis autolea mwito Umoja wa Ulaya kuwa na mshikamano
Papa Francis autolea mwito Umoja wa Ulaya kuwa na mshikamano

Papa Francis leo ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kubaki na mshikamano katika kukabiliana na athari za janga la virusi vya Corona.

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani ametowa mwito huo siku moja kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaojadili mpango mkubwa wa kiuchumi.

Janga la virusi vya Corona limesababisha mivutano mingine katika umoja huo wenye wanachama 27, na kwa mara nyingine kuonekana migawanyiko kati ya nchi tajiri za Ulaya Kaskazini na zile masikini kabisa za upande wa kusini. Kadhalika Papa Francis ameuomba Umoja huo kusali ili ufanikiwe kuuendeleza mshikamano wao wa miaka mingi.

Ni mara ya pili katika kipindi cha siku 10 kwa Papa Francis ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa Umoja wa Ulaya kuzungumzia wasiwasi wake kuhusu Jumuiya hiyo.

April 22, 2020

Merkel Apunguza vizuizi vya corona
Merkel Apunguza vizuizi vya corona

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza hapo jana awamu mpya ya mpango wa mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 unaotokana na virusi vya corona.

Hatua hizo ni pamoja na kuanza pole pole kufunguliwa kwa shule na maduka ya biashara za rejareja, kwa masharti kwamba hatua za kujikinga na maambukizi hayo zitaendelea kuzingatiwa kama vile kuweka nafasi ya umbali wa mita moja na nusu kutoka mtu mmoja hadi mwengine.

Kansela Merkel ameonya kwamba wananchi wa Ujerumani watalazimika kuendelea kuishi na virusi vya corona hadi ipatikane chanjo ya kuweza kujikinga kutokana na virusi hivyo.

Hata hivyo, mipaka itaendelea kufungwa kwa siku 20 zijazo.

April 16, 2020

DRC yaonywa kuhusu maambukizi kuwa mabaya zaidi
DRC yaonywa kuhusu maambukizi kuwa mabaya zaidi

Mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimetoa ombi la jitihada pana zaidi za kuzuia athari mbaya kabisa zinazoweza kusababishwa na kiwango cha juu cha visa vya maambukizi ya virusi vya corona katika mji mkuu Kinshasa.

Kulingana na ripoti ya kitengo kinachosimamia ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi hivyo iliyoonwa na shirika la habari la AFP, kitengo hicho kimesema janga hilo katika mji huo mkuu, linaingia katika awamu ngumu.

Ripoti hiyo imesema kunatarajiwa ongezeko hilo litatokea kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Mei ikisema wanataraji kupata idadi kubwa ya wagonjwa na huenda vituo vya afya vikaelemewa.

Taifa hilo kubwa zaidi kieneo kusini mwa jangwa la Sahara, linalokabiliwa na hali mbaya ya mifumo ya afya, umasikini na makazi mengi ya mabanda katika mji huo mkuu wa Kinshasa.

Ripoti hiyo inafuatia kikao cha wadau wa afya katika kushughulikia janga la COVID-19.

Hadi sasa kumerekodiwa vifo 21 na visa 254 va maambukizi nchini humo.

April 16, 2020

Ufaransa Yaongeza Mwezi Mmoja wa Tahadhari Dhidi Ya Corona....Baada ya Muda Huo Shule Huenda Zikafunguliwa
Ufaransa Yaongeza Mwezi Mmoja wa Tahadhari Dhidi Ya Corona....Baada ya Muda Huo Shule Huenda Zikafunguliwa

Ufaransa imeongeza muda wa kuendelea kuchukua tahadhari za kudhibiti maamukizi ya virusi vya corona hadi Mei 11.

Jumatatu Ufaransa imeripoti vifo 574 vinavyotokana na maambukizi ya virusi hivyo, na kuifanya idadi jumla ya vifo kufikia watu15,000.

Rais Emmanuel Macron amesema ifikapo tarehe hiyo shule zitaanza kufunguliwa.

Hata hivyo, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 wanaohitaji uangalizi maalumu imepungua kwa siku ya tano mfululizo.

Macron amesema kasi ya janga hilo inaanza kupungua na dalili za kudhihirisha hilo ziko wazi. “Mei 11 itakuwa mwanzo wa awamu mpya.

April 14, 2020

Watu 116 walioripotiwa kupona Corona wakutwa tena na maambukizi Korea Kusini
Watu 116 walioripotiwa kupona Corona wakutwa tena na maambukizi Korea Kusini

Watu 116 walioripotiwa kupona Corona awali wamekutwa tena na maambukizi hayo nchini Korea Kusini.

Wiki iliyopita Korea Kusini iliripoti watu 51 ambao tayari walikuwa wamepona kukutwa tena na maambukizi, Serikali nchini humo imeweka wazi kuwa inaangalia mapendekezo madhubuti ya kuzuia maambukizi mapya.

Wataalam wengine wa kiafya wamedai kuwa hali hiyo inaweza ikawa inasababishwa na matatizo wakati wa upimaji au wagonjwa kuachiwa mapema

Mpaka sasa nchi hiyo imeripoti kesi 10,537 na vifo 217 vilivyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona

April 14, 2020

Rais Museven ataka Wenye Nyumba Wasiwafukuze Wapangaji wakati huu wa mlipuko wa Corona
Rais Museven ataka Wenye Nyumba Wasiwafukuze Wapangaji wakati huu wa mlipuko wa Corona

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametoa onyo kwa wapangaji nchini humo na kuwataka wasiwafukuze wapangaji wanaoshindwa kulipa kodi katika wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliana na janga la Corona

Museveni amesema huu sio mwisho wa dunia na kwamba wenye nyumba wanapaswa kuwa wavumilivu na waelewa kwani janga hili litakapoisha, madeni yote yatalipwa

Pamoja na hayo, Rais Museveni pia amewaagiza Polisi nchini humo kuingilia kati pale wanapokuta mpangaji anafukuzwa

Siku chache zilizopita, Rais Museveni alipiga marufuku watu kuendesha magari yao isipokuwa ya kusafirisha mizigo na kutokufunguliwa kwa maduka na kuruhusu biashara ya vyakula pekee.

April 9, 2020

Seneta Bernie Sanders ajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais Marekani
Seneta Bernie Sanders ajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais Marekani

Seneta Bernie Sanders amejiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, huku akiahidi kushirikiana na Joe Biden, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda katika kura za mchujo katika chama cha Democratic.

Bw Sanders amewatolea wito wafuasi wa chama chake cha Democratic kushikamana vilivyo kwa kumshinda Donald Trump katika uchaguzi wa urais ambao umepangwa kufanyika mwezi Novemba.

Katika kuwatangazia wafuasi wake kwamba anajiondoa katika kura za mchujo za chama cha Democratic, Bernie Sanders amemsifu Joe Biden kama "mtu anayeheshimika sana" na kutangaza kwamba atashirikiana na mgombea mwenye msimamo wa wastani ili kuendeleza mpango wake uliozimwa na mrengo wa kushoto.

Baada ya kuelewa kuwa kuna mivutano kati ya kambi hizo mbili, Makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden, mwenye umri wa miaka 77, ameamua kuungana haraka na wafuasi wa Bernie Sanders mwenye umri wa miaka 78.

April 9, 2020

Rais wa Uganda Yoweri Museveni atangaza amri ya kutotoka nje kwa siku 14
Rais wa Uganda Yoweri Museveni atangaza amri ya kutotoka nje kwa siku 14

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametagaza masharti zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona wiki mbili baada ya kupiga marufuku usafiri wa Umma.

Katika hotuba yake kwa taifa iliyopeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni usiku wa Jumatatu Bw. Museveni amepiga marufuku usafiri wa kutumia magari binafsi na boda boda kuanzia saa nne usiku.

Mtu yeyote anayehitaji huduma za dharura za kiafya kama vile kujifungua au kufanyiwa upasuaji anatakiwa kupata idhini kutoka kwa maafisa wa serikali katika ngazi ya Wilaya kabla ya kutoka nyumbani

Wauzaji bidhaa za chakula sokoni watahitajika kuondoka maeneo yao ya biashara hadi pale serikali itakapokamilisha kushughulikia maeneo mapya ya wao kuuzia bidhaa zao .

Rais Museveni pia ameahidi msaada wa chakula kwa watu ambao hawafanyi kazi kutokana na vikwazo vya kukabiliana na covid-19 na hawana uwezo wa kujipatia bidhaa hiyo muhimu.

Bw. Museveni pia ametoa agizo kwa polisi kuwakamata wanasiasa watakaotoa misaada ya chakula kwa jamii na kushtakiwa kwa ''jaribio la mauaji ''

Uganda kufikia sasa imethibitisha kuwa na wagonjwa 33 wa corona na maafisa wanatarajia idadi hiyo kuongezeka.

March 31, 2020

UN yaidhinisha maazimio manne
UN yaidhinisha maazimio manne

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeidhinisha maazimio manne jana, wakati wajumbe wake 15 wakipiga kura kwa kutumia barua pepe kwa mara ya kwanza kutokana na janga la virusi vya corona.

Wajumbe wamepiga kura ujumbe wake wa kulinda amani kuendelea kuwapo katika jimbo la Darfur hadi mwishoni mwa Mei na kuendeleza ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa mataifa nchini Somalia hadi Juni 30.

Wamerefusha muda wa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaoangalia utekelezwaji wa vikwazo dhidi ya Korea kaskazini hadi Aprili 30, 2021, na wamesisitiza umuhimu wa kuunga mkono operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani katika maeneo mbali mbali duniani.

Chombo hicho muhimu cha Umoja wa mataifa kimekuwa kikifanya mikutano kwa njia ya vidio kwa sababu ya ugonjwa wa COVID-19, ambao umeukumba mjini New York , ambako Umoja wa Mataifa una makao yake makuu.

March 31, 2020

Baraza la Seneti lapitisha mpango wa kuupiga jeki uchumi
Baraza la Seneti lapitisha mpango wa kuupiga jeki uchumi

Baraza la Seneti la Marekani limepitisha kwa kauli moja, mpango wa kuupiga jeki uchumi wa nchi hiyo, ili ustahimili madhara ya mripuko wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona.

Baraza la wawakilishi pia linatarajiwa kuuidhinisha mpango huo wenye thamani ya dola trilioni mbili, baadaye wiki hii.

Miongoni mwa mambo mengine, fedha hizo zitasaidia kuimarisha bima kwa watu ambao watapoteza ajira.

Hali kadhalika, zitatumiwa katika sekta ya afya, na majimbo ya nchi hiyo yaliyoathiriwa zaidi na virusi vya corona yatapata msaada wa mabilioni ya dola.

Vile vile makampuni na mashirika madogo na ya kadri yanaweza kuomba mikopo.

Inaelezwa pia kuwa kutoka katika fedha za mpango huo, walipakodi watapatiwa marejesho yao mara moja katika juhudi za kuchochea ufufuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

March 26, 2020

Ndege ya kijeshi ya Urusi yaanguka katika Bahari Nyeusi
Ndege ya kijeshi ya Urusi yaanguka katika Bahari Nyeusi

Shirika la habari la Urusi limeripoti kuwa ndege ya jeshi la nchi hiyo chapa SU-27 ilianguka katika Bahari Nyeusi na kwamba operesheni imeendelea kumtafuta rubani wa ndege hiyo.

Shirika hilo limesema ndege hiyo ilipotea kwenye rada ikiwa umbali wa kilometa 50 kutoka mji wa Feodosia katika rasi ya Crimea, ambayo Urusi imeinyakua kutoka Ukraine.

Wafanyakazi wa uokozi wanasema wamefuata ishara za njia ya mawasialiano ya dharura ya redio, ambayo imesikika mahala ambapo pameelezwa kuwa mbali sana na walipoanzia uchunguzi wao, hii ikiwa ni kwa mujibu wa afisa wa serikali aliyenukuliwa na shirika la habari la Tass.

Imearifiwa kuwa ndege hiyo iliyoanguka ilikuwa katika ujumbe ambao hata hivyo maelezo yake zaidi hayakutolewa.

Shughuli hizo za uokozi znatatizwa na hali mbaya ya hewa

March 26, 2020

Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano kote ulimwenguni
Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano kote ulimwenguni

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano katika mataifa yanayokabiliwa na vita kote ulimwenguni ili kukabiliana na janga la corona.

Guterres amesema kuwa huu ni wakati wa kusitisha mapigano na kuangazia kwa pamoja vita vikali zaidi vya maisha.

Guterres ameongeza kuwa dunia inakabiliwa na adui mmoja ambaye ni ugonjwa wa COVID-19 usiojali uraia wa mtu, kabila, tabaka ama imani.

Amesema wanawake, watoto, walemavu na watu wasiokuwa na makazi pamoja na wale walioko katika maeneo ya vita kote duniani, ndio wanaokabiliwa na hatari zaidi ya kupata hasara kubwa kutokana na virusi hivyo vya corona.

Guterres amesema hayo huku mzozo wa Syrian ukiingia mwaka wake wa 10, Yemen mwaka wa tano na serikali pinzani nchini Libya zikipigana kwa takriban mwaka mmoja sasa

March 24, 2020

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lakwama kuhusu corona
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lakwama kuhusu corona

Duru za kidiplomasia zimesema jana Jumatatu kuwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo halijakutana kwa siku 12 kutokana na mripuko wa virusi vya corona, linakabiliwa na mgawanyiko mkubwa kutokana na azimio lililopendekezwa kuhusu janga hilo na kuandaa mikutano kwa njia ya ''mtandao'' kupigia kura maazimio.

Utata huo unajiri huku viongozi wa dunia wakijaribu kupambana na janga hilo la corona huku mataifa yanayohasimiana ya China na Marekani yakijiingiza katika vita vya maneno na wataalamu wa kimatibabu wakitoa wito wa hatua za pamoja.

Rasimu ya pendekezo hilo iliyoandikwa wiki iliyopita na Estonia, inaangazia ''hofu inayoongezeka kuhusu kuenea pakubwa kwa ugonjwa wa COVID-19, katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa na ambayo huenda ikahatarisha amani na usalama wa kimataifa.''

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanachama wa Baraza hilo la Usalama wamezihimiza nchi wanachama kutilia mkazo kuyasaidia mataifa yanayokabiliwa na hatari zaidi kutokana na virusi hivyo na watu walio katika hali mbaya za kibinadamu.

March 24, 2020

Mkutano wa G7 sasa kufanyika kupitia video
Mkutano wa G7 sasa kufanyika kupitia video

Rais wa Marekani Donald Trump amefuta Mkutano wa viongozi wa mataifa 7 tajiri dunaini G7 na badala yake watazungumza kwa njia ya video kutoa fursa kwa viongozi kushughulikia mripuko wa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi zao.

Mkutano huo uliokuwa uwakutanishe viongozi wa mataifa ya Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Italia, Uingereza na Marekani ulikuwa ufanyike mnamo mwezi Juni katika jimbo la Marekani la Maryland.

Trump pia atakutana na viongozi wa mataifa hayo saba kwa njia ya video mnamo mwezi Aprili na Mei baada ya viongozi hao kufanya mkutano kuhusu mripuko wa virusi vya corona wiki hii.

Kwa hali inavyoendelea, serikali ya Trump inaamini mripuko wa virusi vya corona utaendelea kuwa na athari ulimwenguni hadi majira ya joto

March 20,2020

Mabadiliko makubwa barani Afrika maambukizi ya Corona
Mabadiliko makubwa barani Afrika maambukizi ya Corona

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Afrika Dr. Matshidiso Moeti amewaambia waandishi habari kwamba bara hilo linashuhudia mabadiliko makubwa katika kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Mataifa thelathini na sita kati ya 54 hadi sasa yamesharipoti maambukizi ya virusi hivyo ambayo jumla yake ni 720.

Siku chache Chad na Niger zilitangaza kuthibitisha maambukizi yake ya kwanza.

Na kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kikiwa kimeripotiwa wiki tatu zilizopita katika mataifa yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara.

Mataifa mengine zaidi barani humo yametangaza kufunga mipaka yake kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo katika bara lenye idadi ya watu wapatao bilioni 1.3.

Moeti amesema haamini kwamba idadi kubwa ya walioambukizwa barani humo wameshindwa kutambuliwa lakini amekubali kwamba kuna upungufu wa vifaa vya kufanyia vipimo vya virusi hivyo vya corona.

March 20,2020

Wauguzi Corona Kenya waanzisha mgomo
Wauguzi Corona Kenya waanzisha mgomo

Wauguzi wanaofanya kazi katika wodi iliyotengwa kwa watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Kenya wameanza mgomo baridi kulalamikia kile wanachodai kuwa ukosefu wa vifaa vya kujikinga na mafunzo ya kutosha.

Hospitali ya Mbagathi katika mji mkuu wa Nairobi, ni moja ya hospitali zilizo na wodi ya kutibu wagonjwa waliombukizwa virusi hivyo hatari.

Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Kenya,Seth Panyako amesema kwamba wauguzi watarejea kazini ikiwa watapewa mavazi maalum na mafunzo ya jinsi ya kuwashughulikia wagonjwa.

Hospitali ya ya Mbagathi inawazuilia watu 22 ambao walisafiri na mgonjwa wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya corona ambapo Kenya kwa sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwatafuta wengine waliofuatana na watu watatu waliothibitishwa kuambukizwa vitrusi vya corona.

March 17, 2020

Rais Vladimir Putin asaini mpango marekebisho ya katiba.
Rais Vladimir Putin asaini mpango marekebisho ya katiba.

Suala la kuifanyia marekebisho katiba na mustakbali wa kisiasa wa Rais Vladimir Putin wa urusi ni jambo lililopewa uzito miongoni mwa matukio ya kisiasa ya hivi karibuni huko urusi .

Kuhusiana na suala hilo, Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo mwishoni mwa wiki amesaini mpango wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.

Lakini Kura ya maoni itafanyika baada ya Mahakama ya Katiba ya urusi kuidhinisha mfumo wa utekelezaji wa marebisho hayo ya katiba.

Marekebisho yanayotazamiwa katika katiba ya urusi yatapigiwa kura na yataweza kutekelezwa iwapo wananchi watayaunga mkono kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura.

March 17, 2020

Waasi washambulia na kuua raia nchini Cameroon
Waasi washambulia na kuua raia nchini Cameroon

Wanajeshi watano na raia wane wamefariki dunia baada ya Waasi kushambulia kituo cha polisi kilichoko wilayani Galim magharibi mwa Cameroon.

Taarifa zimesema hujuma hiyo ya usiku wa kuamkia Jumapili ilitekelezwa na waasi takriban 20 wakiwa wamepanda pikipiki katika mkoa huo ambao wakaazi wake wengi wanazungumza Kifaransa.

Gavana wa eneo la magharibi mwa Cameroon Awa Fonka Augustine amesema wanawatafuta waasi waliotekeleza hujuma hiyo.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 3,000 wameuawa nchini Cameroon tangu mwaka 2017 na wengine 530,000 kukimbia makazi yao kufuatia kuanza uasi katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza.

March 09, 2020

Rais wa Uturuki asema jeshi liko tayari iwapo makubaliano yatakiukwa Idlib
Rais wa Uturuki asema jeshi liko tayari iwapo makubaliano yatakiukwa Idlib

Rais wa Uturuki amesema kuhusu makubaliano ya kusitishwa mapigano huko Idlib jeshi lipo tayari iwapo makubaliano yatakiukwa.

Rais wa Uturuki Recep Tayyıp Erdoğan asema kwamba jeshi la Uturuki halitosita kuanza upya operesheni yake iwapoa jeshi la Assad litakiuka makubaliano Idlib.

Kwa mara nyingine rais Erdoğan amekumbusha kuwa kamwe Uturuki haina lengo la kuhujumu ardhi ya Syria katika operesheni zake.

Kwa mujibu wa rais Erdoğan watoto na wanawake ndio waathirika wa kwanza katika mapigano yanayoendelea nchini Syria

March 09, 2020

Saudi Arabia imezuia wageni wanaoingia nchini humo
Saudi Arabia imezuia wageni wanaoingia nchini humo

Serikali ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini, ikiwemo wanaotembelea miji ya Makka na Madina.

Mamilioni ya watu huingia Saudia mwaka mzima kufanya ibada ya Umra, na wengi zaidi huingia kwa pamoja kufanya ibada ya Hija.

Tofauti na Hija, Umra hufanyika katika kipindi chochote cha mwaka, na kwa sasa marufuku hiyo inawalenga mahujaji raia wa nchi za nje wanaotaka kwenda kuhiji.

Bado haijulikani kama ibada ya Hija, ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai kama itaathirika na zuio hilo pamoja na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.

February 28, 2020

Nzige wa jangwani wavamia Kongo
Nzige wa jangwani wavamia Kongo

Kundi la nzige wa jangwani limeingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wadudu hao hatari kuonekana katika taifa la Afrika ya Kati tangu mwaka 1944.

Shirika hilo la chakula FAO aidha limeonya juu ya Tishio kubwa la njaa katika mataifa ya Afrika Mashariki baada ya kuvamiwa na nzige hao.

Kenya, Somalia na Uganda zimekuwa zikipambana na wadudu hao, katika mripuko mbaya kabisa wa nzige ambao maeneo kadhaa ya ukanda huo yalishuhudia miaka 70 iliyopita.

Umoja wa Mataifa umesema nzige hao wa jangwani pia wameonekana katika siku za karibuni wamefika Sudan Kusini, taifa ambalo nusu ya idadi ya watu wake wanakabiliwa na njaa baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

February 28, 2020

Watu 9 wauawa kwa risasi mjini Hanau, Ujerumani
Watu 9 wauawa kwa risasi mjini Hanau, Ujerumani

Watu tisa wameuawa baada ya mtu mmoja kufyatua risasi katika maeneo mawili tofauti mjini Hanau katika jimbo la Hessen nchini Ujerumani

Mwendesha mashitaka wa serikali katika eneo hilo amesema mapema leo kuwa mamlaka zinafanya uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo yaliyofanywa katika baa mbili zinamovutwa shisha katikati mwa mji wa Hanau na kisha katika baa nyingine kwenye mji wa Kesselstadt.

Polisi nchini Ujerumani imesema mtuhumiwa wa mauaji hayo katika mji ulio magharibi mwa ujerumani wa Hanau alikutwa amekufa nyumbani kwake mapema leo. Polisi wa eneo hilo wamesema timu maalumu ya wataalamu ilikuta pia mwili wa mtu mwingine katika nyumba ya mtuhumiwa, lakini hakuna dalili ya mtu huyo kuhusika kwenye mauaji hayo. Hakuna majeruhi walioripotiwa kutokana na tukio hilo.

Awali mtuhumiwa wa shamulio hilo anayehusishwa na siasa kali za mrengo wa kulia alituma video kwa njia ya mtandao yenye urefu wa karibu saa moja akidai kuwa Ujerumani inaongozwa na taasisi ya siri yenye mamlaka makubwa. Katika vidio hiyo alitoa pia kauli dhidi ya wahamiaji kutoka nchi za Kiarabu na Uturuki.

February 21, 2020

Sudan Kusini wametangaza kuunda serikali ya muungano
Sudan Kusini wametangaza kuunda serikali ya muungano

Viongozi wanaohasimiana nchini Sudan Kusini wametangaza kuwa wamekubaliana kuunda serikali ya muungano, ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kumalizika muda wa mwisho uliowekwa.

Tangazo hilo ni hatua kubwa katika kupatikana kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenywe nchini humo vilivyodumu kwa miaka mitano na kuwaua karibu watu 400,000 na kuliharibu kabisa taifa hilo changa kabisa duniani.

Kiongozi wa upinzani Riek Machar amesema mjini Juba kuwa yeye na Rais Salva Kiir wamekubaliana kuwa baada ya kuundwa serikali hiyo watayatatua masuala mengine yaliyobaki. Amesema ana matumaini kuwa watayashughulikia yote.

Kiir amesema serikali mpya itaundwa Jumamosi, akiongeza kuwa mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuleta amani.

Amesema atamteuwa Machar kuwa makamu wake wa kwanza wa rais. Rais Kiir pia amesema mpangilio wa usalama, mojawapo ya masuala muhimu, utatatuliwa baada ya kuundwa serikali. Ulinzi wa Machar na wengine kutoka upinzani utakuwa chini ya wajibu wake.

February 21, 2020

Vikosi vya Syria Vyateka sehemu ya mkoa wa Aleppo
Vikosi vya Syria Vyateka sehemu ya mkoa wa Aleppo

Vyombo vya habari nchini Syria vinasema vikosi vya serikali vimepiga hatua muhimu na kuyateka maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wa waasi katika mkoa wa Aleppo ulioko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Mafanikio haya ya serikali yametangazwa siku moja kabla mazungumzo mapya kati ya Urusi na Uturuki kuhusiana na kuongezeka kwa mapigano katika eneo hilo.

Hatua hii ya serikali ya Syria imeutatiza ushirikiano kati ya Uturuki na Urusi, ambazo wanaunga mkono pande tofauti katika mzozo huo wa miaka tisa, ingawa zinashirikiana katika kutafuta suluhisho la kisiasa.

Kulingana na wanaharakati, hapo jana ndege za kivita za Urusi ziliishambulia miji kadhaa ukiwemo wa Anadan ambao baadaye ulitekwa na vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na wanamgambo wa Iran.

Duru za kijeshi zimearifu kwamba wapiganaji wa upinzani wameondoka kutoka Anadan na mji wa Haritan.

February 18, 2020

China yasajili idadi ndogo ya maambukizi ya virusi vya Corona
China yasajili idadi ndogo ya maambukizi ya virusi vya Corona

Maafisa wa China wanasema wanayo matumaini kuwa kiwango cha maambukizi mapya ya homa inayoambukizwa na virusi vya Corona kinashuka.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa wengi wanaoambukizwa hivi sasa hawatakufa kutokana na homa hiyo, bali wataonyesha dalili zisizo kali sana.

Idadi ya visa vipya vya maambukizi vilivyosajiliwa leo Jumanne nchini China ni 1,886, ambayo ni ndogo kwa siku moja nchini China Bara tangu mwanzoni mwa mwezi huu.

Ripoti iliyochapishwa na maafisa wa afya wa China jana Jumatatu, ilisema asilimia 80 ya wagonjwa wapya hawakuonyesha ishara mbaya, na hatari ya kifo iliongezeka kulingana na umri wa mtu, na hali yake ya afya kabla ya kuambukizwa.

Mamlaka za China zinasema ahueni inayoshuhudiwa ni ushahidi kuwa hatua walizozichukuwa tangu kuzuka kwa homa hiyo zinaanza kuzaa matunda.

February 18, 2020

Papa akataa wanaume waliyooa kuwa mapandre.
Papa akataa wanaume waliyooa kuwa mapandre.

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis jana alikataa pendekezo kutoka kwa maaskofu wa eneo la Amazon ambalo lingeruhusu watu waliooa kuwa mapadre na wanawake kuwa wahudumu wa kike kanisani, ili kujaza upungufu wa watu hao katika eneo hilo.

Jibu la Papa, lilikuwa linasubiriwa kwa hamu kubwa lakini alichagua kutohusisha suala la ndoa katika waraka wake wenye vipengee 111 chini ya kichwa cha habari Wapenzi Amazon.

Francis alitoa wito wa wamisionari zaidi kutumwa katika eneo la Amazon na kuwahimiza maaskofu wote kutoka Amerika ya kusini, kuwa wajitolea zaidi katika kuwahimiza wale ambao wanataka kwenda likizo ya umisionari kuamua kwenda katika eneo la Amazon.

February 14, 2020

Mahakama yakataa rufaa ya Rais Peter Mutharika
Mahakama yakataa rufaa ya Rais Peter Mutharika

Mahakama ya Katiba nchini Malawi imekataa rufaa iliyokatwa na Rais Peter Mutharika ya kupinga hukumu ya mahakama hiyo kumfutia ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa Mei 2019.

Februari 3, mwaka huu mahakama hiyo ilibatilisha ushindi wa Rais Mutharika kwa kura chache dhidi ya mpinzani wake, kwa maelezo kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na ukiukwaji wa taratibu, na kuamuru uchaguzi mpya kufanyika ndani ya siku 150.

Aidha, mahakama hiyo umetupilia mbali madai ya tume ya taifa ya uchaguzi kuwa kufanyika kwa uchaguzi wa marudio itakuwa ni gharama kubwa sana.

Akitoa uamuzi wa mahakama, Jaji Dingiswayo amesema demokrasia ina gharama zake, na haki za binadamu ni muhimu.

Uamuzi wa mahakama kumfutia ushindi Mutharika ulifikiwa baada ya uchunguzi uliofanyika kubaini kuwepo kwa matumizi ya wino wa kufuta maandishi (correctional fluid & Tippex) vilivyotumika kubadilisha takwimu pamoja na matumizi ya nakala bandia za matokeo.

February 14, 2020

Rais wa China atembelea wagonjwa wa virusi vya Corona
Rais wa China atembelea wagonjwa wa virusi vya Corona

Rais wa China, Xi Jinping jana jumatatu amewatembelea wagonjwa wa virusi vya Corona pamoja na maafisa wa afya ambao wanawahudumia wagonjwa hao.

Xi alionekana amevalia kitambaa cha kufunika uso kwa ajili ya kujikinga na pia alipima afya yake.

Huku akiviita virusi vya Corona kama ''janga'', Xi amesema hatua kali zaidi zitachukuliwa kwa ajili ya kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Rais Xi amemteua Waziri Mkuu Li Keqiang kuongoza kundi la wafanyakazi litakaloshughulikia mripuko wa virusi hivyo na mwezi uliopita Li aliutembelea mji wa Wuhan ambako virusi hivyo vilianzia.

Wakati huo huo, timu ya wataalamu wa Shirika la Afya duniani imeelekea Beijing kuchunguza mripuko wa virusi vya Corona. Hadi sasa virusi hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 900 na wengine zaidi ya 40,000 wameambukizwa.

Chanzo dw

February 11, 2020

Hakuna tena kuchelewesha kuunda serikali ya Sudan Kusini
Hakuna tena kuchelewesha kuunda serikali ya Sudan Kusini

Mataifa ya Afrika Mashariki yamesema serikali ya kugawana madaraka haipaswi tena kuchelewesha kuundwa nchini Sudan Kusini, licha ya mazungumzo kati ya viongozi hasimu kukwama.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar wanatakiwa kuunda serikali ifikapo tarehe 22 ya mwezi huu.

Kuundwa kwa serikali mpya kumecheleweshwa mara mbili mwaka uliopita na muda wa siku 100 ulioongezwa unafikia mwisho Februari 22 mwaka huu.

Taarifa ya nchi nane wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Pembe ya Afrika, IGAD, imesema hapahitajiki tena wala haiwezakani kuongeza muda katika hatua hii ya mchakato wa amani.

Hapo Jana Kiir na Machar walikutana nchini Ethiopia pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, pamoja na viongozi wa nchi jirani wa Uganda, Yoweri Museveni na Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hambok, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa IGAD, lakini hawakufikia muafaka wa kutatua mzozo kuhusu idadi ya majimbo.

Chanzo:rfi

February 11, 2020

Kiongozi wa Al-Qaeda auawa Marekani
Kiongozi wa Al-Qaeda auawa Marekani

Marekani imemuua kiongozi wa Al-Qaeda katika eneo la Rasi ya uarabuni, Rais Donald Trump ameeleza.

Qasim al-Raymi aliyeongoza kikundi cha Jihad tangu mwaka 2015, aliuawa wakati wa operesheni ya majeshi ya Marekani nchini Yemen, Ikulu ya Marekani imeeleza.

Kiongozi wa wapiganaji wa Jihad amekuwa akihusishwa na mfululizo wa mashambulizi dhidi ya maslahi ya nchi za Magharibi katika miaka ya 2000.

Tetesi kuhusu kifo cha al- Raymi kwa shambulizi la Marekani zilianza kusambaa mwishoni mwa mwezi Januari. Katika kujibu hilo kundi hilo lilitoa ujumbe wa sauti ukiwa na sauti ya al -Raymi tarehe 2 mwezi Februari ukisema kuwa wao ndio waliotekeleza shambulio la risasi kwenye kambi ya jeshi la wana maji wa Marekani huko Pensacola, Florida.

Shambulio hilo lilifanyika mwezi Desemba, na ujumbe huo huenda ulirekodiwa mapema.

Chanzo; BBC. Feb. 7

February 7, 2020

Ukeketaji kupoteza mabillioni ya fedha
Ukeketaji kupoteza mabillioni ya fedha

Umoja wa Mataifa umesema jana kuwa ukeketaji wa wanawake unadhoofisha uchumi wa mataifa mengi.

Umoja huo umesema hayo ulipozindua kifaa cha kusaidia katika kutathmini gharama ya kuwatibu wasichana na wanawake ambao wamejeruhiwa kufuatia ukeketaji.

Kifaa hicho kimezinduliwa February 6 ambayo ni siku ya kimataifa ya kupambana na ukeketaji wa wanawake, na kitashughulikia nchi 27, nyingi zikiwa Afrika.

Shirika la Afya Duniani-WHO, limekadiria kuwa itagharimu dola bilioni 1.4 kila mwaka kuyatibu madhara yote yanayotokana na ukeketaji wa wanawake.

Takriban wanawake na wasichana milioni 200, kote ulimwenguni wamekeketwa, hali inayosababisha matatizo mbalimbali ya kiafya yakiwemo ya kiakili na mwilini.

February 7, 2020

Matokeo ya Rais Peter Mutharika yafutwa Malawi
Matokeo ya Rais Peter Mutharika yafutwa Malawi

Malawi imeyafuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Mei 2019, uliompa ushindi Rais Peter Mutharika.

Akitoa uamuzi wake Jaji Healey Potani alisema ingawa chaguzi zote zina mapungufu, uchaguzi uliopita ulighubikwa na hitilafu za kimfumo zilizokithiri kiasi cha kuweza kubadilisha matokeo.

Mahakama hiyo ilisema matokeo ya uchaguzi huo yamebatilishwa, na kuitaka tume ya uchaguzi kuandaa uchaguzi mwingine katika muda wa siku 150.

Katika uchaguzi huo, Rais Mutharika aliyekuwa akiwania muhula wa pili alipata ushindi mdogo wa asilimia 38, huku mpinzani wake mkuu Lazarus Chakwera akikusanya asilimia 35.

Usalama umeimarishwa kote nchini humo baada ya uamuzi huo wa mahakama.

February 4, 2020

Rais wa pili wa Kenya Afariki Dunia
Rais wa pili wa Kenya Afariki Dunia

Daniel Arap Moi, rais wa pili wa Kenya ameaga dunia leo Jumanne. Kifo chake kimetangazwa na Rais Uhuru Kenyatta, katika tangazo lililorushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa.

Tangazo hilo kutoka Ikulu limesema kuwa mzee Moi, hata baada ya kuondoka madarakani aliendelea kulitumikia taifa la Kenya na Afrika kwa kuwafundisha viongozi wa Kenya na nje ya Kenya, akiendelea kushiriki kwenye maendeleo ya miradi mbalimbali na kazi za misaada akiihubiri amani, upendo na umoja barani Afrika na duniani.

Mzee Moi alizaliwa Septemba 2, 1924 na alitawala Kenya kwa miaka 24 kutoka 1978 mpaka 2002.

February 4, 2020

Gambia wataka Rais wake Ajiuzulu
Gambia wataka Rais wake Ajiuzulu

Gambia imeendelea kukabiliwa na hali ya sintofahamu, baada ya maelfu ya watu kuingia mitaani wakidai rais Adamu Barrow ajiuzulu.

Maandamano hayo yamefanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul huku Makabiliano kati ya waandamanaji na polisi yalishuhudiwa.

Idadi ya waliopoteza maisha au kujeruhiwa haijajulikana lakini mkurugenzi wa hospitali kuu ya Serrekunda mjini Banjul, Kebbah Manneh, amesema kwamba watu watatu wamepoteza maisha katika makabiliano hayo ,Taarifa ambayo imekanushwa na serikali kupitia msemaji wake, Ebrima Sankareh.

January 28 2020

Boko Haram Kuishambulia Chad
Boko Haram Kuishambulia Chad

Imeelezwa kuwa Jeshi la Chad limeendelea kulengwa katika mashambulizi mbalimbali yanayotekelezwa na makundi ya watu wenye silaha, huku raia wakihofia usalama wao.

Askari sita wameuwawa katika shambulio jipya linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram karibu na Kisiwa cha Tetewa, kinachopatikana kwenye Ziwa Chad, eneo ambalo machafuko yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Kwa miezi kadhaa, wanamgambo wa Kiislamu wameongeza mashambilizi karibu na Ziwa Chad, eneo kubwa la visiwa lililojaa maji kwenye mpaka wa Chad, Cameroon, Niger na Nigeria.

January 28 2020

Zimbabwe kukumbwa na maandamano makubwa
Zimbabwe kukumbwa na maandamano makubwa

Kiongozi mkuu wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa ametangaza maandamano zaidi anayosema, yanalenga kushinikiza mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini humo.

Chamisa amesema maandamano hayo yanayoandaliwa na chama chake cha MDC, ndio njia pekee ya raia wa nchi hiyo kufikia malengo yao, na kuwaondoa katika mateso wanayopitia nchini ya rais Emmerson Mnanganagwa.

Tangu alipoingia madarakani, uongozi wa rais Mnangangwa umeendelea kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na kisiasa, wakati huu mataifa ya Magharibi yakiendelea kuiwekea vikwazo vya kiuchumi taifa hilo la Kusini mwa bara la Afrika.

Wazimbabwe wengi wanaonekana kuwa katika hali mbaya zaidi kuliko hapo mwaka 2009, pale taifa hilo la kusini mwa Afrika lilipoachia sarafu yake isiyo na thamani na kuanza kutumia sarafu mbali mbali hususan dola ya marekani.

January 23, 2020

Burundi kumpa Rais mstaafu fungu nono
Burundi kumpa Rais mstaafu fungu nono

Bunge la Burundi limeidhinisha sheria inatakayompa rais mstaafu kitita cha faranga bilioni za Burundi sawa na Dola laki 5 za Marekani.

Lakini Kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa amesema fedha hizo ni nyingi sana ila hiyo itamfanya rais mstaafu asione umuhimu wa kugombea tena

Sheria hiyo iliyofafanuliwa bungeni na waziri wa sheria inaagiza pia rais atakapostaafu atakuchukuliwa kwa hadhi ya makamu wa rais kwa kipindi cha miaka 7.

Agathon Rwasa aliye pia Naibu Spika wa bunge amesema huenda chama tawala chenye wingi wa wabunge kilikusudia kuepusha kumpa maisha mazuri rais Baada ya kustaafu ili asiwe na nia ya kugombea tena lakin usalama wa nchi ni muhimu kuliko marupurupu hayo.

January 23, 2020

Nchi tatu zatia saini mpango wa nyuklia wa Iran
Nchi tatu zatia saini mpango wa nyuklia wa Iran

Nchi tatu za Umoja wa Ulaya zimekitumia kipengele cha kusuluhisha mizozo katika makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, yaliyosainiwa mwaka 2015.

Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ambazo zimeweka saini makubaliano hayo, zimesema zimechukua hatua hiyo baada Iran kukiuka mara kwa mara ukomo wa kurutubisha madini ya urani uliowekwa katika makubaliano yao.

Hata hivyo nchi hizo za Ulaya zimesisitiza kwa mara nyingine kuwa zinaendelea kuyaunga mkono makubaliano hayo, zikipinga shinikizo la utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kuzitaka kutounga mkono.

Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka jana, na kurejesha vikwazo vilivyokuwa vimelegezwa dhidi ya Iran ambapo Uamuzi huo wa Marekani umeongeza mvutano kati yake na Iran, ambao ulikaribia kuingia katika vita kamili baada ya Marekani kumuuwa jenerali maarufu wa Iran, Qasem Soleimani, mwanzoni mwa mwezi huu.

January 15,2020

Rais wa Uturuki kumchukulia atua Khalifa Haftar
Rais wa Uturuki kumchukulia atua Khalifa Haftar

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametishia kumchukulia hatua za kijeshi mbabe wa kivita nchini Libya, Khalifa Haftar, ikiwa ataendelea kuishambulia serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa kimataifa.

Haya yanajiri baada ya Haftar kuondoka katika mkutano wa upatanishi mjini Moscow hapo jana, bila kusaini makubalino ya kusitisha mapigano, ambayo kiongozi wa serikali ya mjini Tripoli ameyaridhia.

Akizungumza na wabunge wa chama chake mapema leo, Erdogan ametishia kumpa funzo Haftar na kusema atashiriki katika mkutano mwingine kuhusu amani nchini Libya, ambao utafanyika Jumapili ijayo mjini Berlin,nchini Ujerumani, ukizishirikisha pia Ufaransa, Uingereza na Italia, na mataifa ya kiarabu kama Misri, Algeria na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Uturuki imepeleka vikosi nchini Libya kuiimarisha serikali ya waziri mkuu Fayez al-Sarraj, na Rais Erdogan amesema vitabaki huko hadi pale utulivu utakapopatikana nchini humo.

January 15,2020


Radio Uhai 94.1 FM Tabora Sauti ya Tumaini

© Radio Uhai